Mbunge Ngorongoro Aanzisha Mfuko wa Elimu Kuwasaidia Wanafunzi 280 Wasio na Uwezo

Na 

Mwandishi wetu ,

ARUSHA.

Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro mkoani Arusha, Mheshimiwa Yannick Ndoinyo, ameanzisha mfuko maalumu wa elimu utakaowanufaisha wanafunzi 280 kutoka wilayani humo, wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini na zisizo na uwezo wa kuwapeleka watoto wao shule za sekondari.

Akizungumza machi 31,2026 katika mahojiano maalum na Yawhe FM, Mheshimiwa Ndoinyo amesema hatua hiyo imelenga kukabiliana na changamoto kubwa ya kipato inayowakabili wakazi wengi wa Wilaya ya Ngorongoro, ambao kwa kiasi kikubwa hutegemea ufugaji kama chanzo chao kikuu cha maisha.

 Pia Ameeleza kuwa lengo kuu la mfuko huo ni kuhakikisha watoto wa jamii ya wafugaji wanapata haki yao ya msingi ya elimu, na hivyo kuwa na fursa sawa ya kufikia ndoto zao za maisha kupitia masomo.

Aidha, Mheshimiwa Ndoinyo ametoa wito kwa jamii kushirikiana na ofisi ya mbunge ili kuhakikisha mfuko huo unawafikia wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji, na kuongeza kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea ushirikiano wa wadau wote wa elimu.

Kuhusu uwazi katika mchakato wa kuwapata wanufaika, amesema ofisi yake inashirikiana kwa karibu na kamati za maendeleo za kata, maafisa elimu wa kata pamoja na walimu wakuu wa shule za msingi ili kuhakikisha wanafunzi wanaochaguliwa wanastahili na hakuna udanganyifu wowote unaojitokeza.



 

0/Post a Comment/Comments