Na
Mwandishi wetu ,
Ngorongoro.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ngorongoro, Ally Joseph Karanjai, ameahidi kumsaidia mtoto mwenye changamoto za kifamilia kurejea shuleni kwa kumpatia mahitaji yote muhimu ya masomo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, ili kuhakikisha anatimiza ndoto zake za kielimu.
Akizungumza machi 30,2026 katika mahojiano maalum na yahwe fm Karanjai amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo, hali ya elimu kwa sasa imeimarika ambapo watoto wengi wanahudhuria masomo ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Amesema jukumu la viongozi na wazazi ni kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyumbani bila sababu, hasa ikizingatiwa kuwa serikali imeondoa ada za masomo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
“Kwa sasa elimu ni bure, kilichobaki ni mahitaji madogo kama sare za shule, madaftari na matumizi mengine ya kawaida ambayo wazazi wanapaswa kuyatimiza,” amesema Karanjai
Aidha, Karanjai ameahidi kusaidia watoto wanaokosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kifamilia kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo sare za shule, vifaa vya kujifunzia pamoja na mahitaji mengine ya msingi.
Ameeleza kuwa msaada huo hautakuwa kwa mtoto mmoja tu bali utaangalia uwezekano wa kusaidia watoto wengine watakaobainika kuwa na uhitaji ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa elimu.
Katika hatua nyingine, amewapongeza viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani na wadau wa ustawi wa jamii kwa juhudi wanazozifanya kuhakikisha watoto wanarudi na kubaki shuleni.
Karanjai amehitimisha kwa kutoa wito kwa wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi na elimu ya watoto wao, akisisitiza kuwa kila mtoto ana ndoto na uwezo wa kufanikiwa endapo atapatiwa fursa ya kusoma.


Post a Comment