Arusha Yafikia Asilimia 30 ya Umeme, Serikali Yasisitiza Utekelezaji Miradi



Na 

Bora Mustafa,

Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Modest Mkude, amesema dhamira ya Serikali chini ya Rais ni kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wote kuanzia ngazi ya wilaya, kata hadi vijiji na vitongoji.

Amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 180 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kusambaza umeme, pamoja na shilingi bilioni 200 zilizotengwa kwa ajili ya kununua vyombo vya usafirishaji vitakavyosaidia kurahisisha utekelezaji wa miradi hiyo nchini.

Mkude ameeleza Leo April 13,2026 kuwa shughuli za utoaji wa umeme zinaendelea katika mikoa mbalimbali, huku mkoa wa Arusha ukiwa na kiwango cha upatikanaji wa umeme cha takribani asilimia 30 kwa sasa.

Amesisitiza kuwa viongozi waandamizi wanaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa wakati na kwa ufanisi, sambamba na mpango wa Serikali wa kufikisha umeme katika vijiji na vitongoji vyote.

Aidha, amewataka watendaji kutumia vizuri magari yaliyotolewa na Serikali yenye thamani ya mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kusimamia na kurahisisha utekelezaji wa miradi ya umeme.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Kisika

 amesema kuwa mkoa huo una vituo vitatu vikuu vya umeme ambavyo ni Njiro, Lemugur na Karatu.

Amesema kwa sasa kuna ziada ya umeme ambapo takribani asilimia 30 pekee ndiyo inayotumika huku asilimia 60 ikiwa bado haijatumika, hali inayotoa fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika mkoa huo.

Kisika ameongeza kuwa mkoa wa Arusha una jumla ya wilaya saba zinazopata huduma ya umeme, vijiji 368 pamoja na mitaa 54. Pia, kupitia miradi ya REA, zaidi ya shilingi bilioni 99 zimetumika kusambaza umeme vijijini na mijini.

Amesema kati ya vitongoji 10,005 vilivyopo, vitongoji 945 tayari vimefikiwa na huduma ya umeme, huku takribani vitongoji 560 bado havijapata huduma hiyo.

Kwa mwaka wa fedha uliopita, TANESCO imepokea zaidi ya shilingi bilioni 19 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya umeme, huku idadi ya wateja ikiwa imefikia zaidi ya laki tatu na elfu themanini (380,000).

Katika kuboresha utendaji kazi, wafanyakazi wameendelea kupewa vitendea kazi muhimu ikiwemo magari makubwa mawili, magari aina ya Land Cruiser manne pamoja na bajaji tano kwa ajili ya kurahisisha usimamizi wa shughuli za umeme.







0/Post a Comment/Comments