Na
Bora Mustafa,
Arusha.
Taasisi ya Waandishi wa Habari ya Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC) imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini kuhusu uandishi wa habari wakati wa migogoro unaozingatia usalama binafsi na kulinda amani ya jamii.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Februari 11,2026 yamehusisha waandishi kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Mara, Manyara, Mbeya na Arusha, huku yakidhaminiwa na shirika la kimataifa la wanahabari la Press Unlimited.
Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, amewataka wanahabari wanaokwenda kuripoti matukio ya migogoro kuzingatia tahadhari za kiusalama na kuepuka kupendelea upande wowote. Amesema kuwa uandishi wa habari za upande mmoja ambazo hazizingatii maadili na maslahi mapana ya umma umekuwa ukichochea migogoro katika jamii.
“Tujiulize habari ina madhara gani au faida gani kwa jamii. Tusiwe na upande katika habari na tuzingatie tahadhari za kiusalama, hususan tunapotumia vyombo vya kidijitali na katika usalama binafsi,” amesema Juma.
Hata hivyo, amewakumbusha wanahabari kufanya upembuzi yakinifu wa kina kabla na baada ya kuandika habari ili kuhakikisha taarifa wanazozitoa hazileti madhara yasiyokusudiwa kwa jamii.
Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea John Sendodo, ametoa mada kuhusu sheria mbalimbali zinazohusu tasnia ya habari, aliwataka wanahabari kuzijua na kuziheshimu sheria hizo hata kama zina mapungufu. Amezitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 pamoja na Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni.
“Kuna sheria kadhaa ambazo ni lazima mzijue. Zisomeni na kuzitambua ili muweze kutekeleza wajibu wenu bila kuvunja sheria,” amesema Sendodo, ambaye pia anafanya kazi na shirika la kimataifa la Protection Africa.
Aidha, amefafanua vifungu mbalimbali vya sheria hizo pamoja na mikataba ya kimataifa inayohusu uhuru na wajibu wa wanahabari.
Pia , Mmiliki wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha Fanikiwa kilichopo Arusha, Joseph Mayagilla, amewataka wanahabari kuzingatia maadili ya taaluma yao wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Amesema kumekuwepo na ongezeko la uandishi usiozingatia maadili, jambo linaloweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.
Mayagilla alisisitiza umuhimu wa kurejesha na kuimarisha madawati maalum katika vyombo vya habari, ikiwemo madawati ya uchunguzi, amani na maendeleo, pamoja na uchumi, ili yaongozwe na waandishi wabobezi na kuongeza ubora wa maudhui.
Kwa upande wa afya ya akili, Mtaalamu wa Saikolojia Ester Cornelio aliwataka wanahabari wanaokabiliwa na msongo wa mawazo kutafuta msaada wa kitaalamu badala ya kujifungia au kutumia pombe na sigara kama njia ya kukabiliana na changamoto hizo.
“Msongo wa mawazo hauondoki kwa kunywa pombe kupita kiasi au kuvuta sigara. Suluhisho ni kufika kwa wataalamu wa ushauri nasaha na kupata tiba stahiki,” amesema Cornelio.
Ameongeza kuwa wanaume wengi wamekuwa wahanga wa sonona kwa sababu hawazungumzi matatizo yao tofauti na wanawake.
Wakichangia mada katika mafunzo hayo, wanahabari Tausi Mbowe, Meneja wa Dawati la Kidijitali wa Star TV, na Anthony Mayunga kutoka Serengeti Media, wamesisitiza umuhimu wa maadili ya uandishi pamoja na kuimarisha uelewa wa sheria na afya ya akili kwa wanahabari.
Mbowe ameshauri kuwepo kwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwajengea wanahabari uwezo wa kukabiliana na changamoto za kisheria na msongo wa mawazo.
Aidha, Elizabeth Nyivambe kutoka Mbeya, Muta Robert wa Geita na Zakaria Mtigandi wa Manyara walieleza umuhimu wa kuendelezwa kwa mafunzo hususan katika matumizi sahihi ya mitandao na usalama wa wanahabari wanaporipoti migogoro.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yamelenga kuwajengea wanahabari uwezo wa kuripoti migogoro kwa weledi, kuzingatia maadili, sheria na usalama wao binafsi, huku wakichangia kudumisha amani na mshikamano katika jamii.





Post a Comment