Waziri Makonda Akagua Miradi ya Maendeleo Jijini Arusha , Amesisitiza Ubora na Uharaka wa Utekelezaji.



Na 

Bora Mustafa, 

Arusha.


 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mhe. Paul Christian Makonda, amefanya  ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jijini Arusha.

Ziara hiyo ilihusisha ukaguzi wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Stendi ya Mabasi unaotekelezwa katika eneo la Bondeni City, ambapo viongozi hao walipata fursa ya kujionea hatua za utekelezaji na kutoa maelekezo kwa wakandarasi.


Akizungumza katika eneo la ujenzi wa stendi hiyo, Mhe. Makonda ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa usimamizi thabiti na utendaji kazi mzuri katika kusimamia miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa uwepo wa viongozi wa mkoa katika maeneo ya miradi mara kwa mara una mchango mkubwa katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.


Aidha, Waziri Makonda amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati uliopangwa na kwa kuzingatia viwango vya ubora, ili stendi hiyo iweze kutoa huduma bora kwa wananchi na wageni wa Jiji la Arusha.


Katika hatua nyingine, ameuagiza uongozi wa mkoa kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa mipango miji ili kuchangamkia fursa zitakazotokana na mradi huo, ikiwemo ujenzi wa maeneo ya shughuli za kiuchumi yatakayosaidia kuongeza ajira na kukuza uchumi wa jiji.


Sambamba na hilo, Mhe. Makonda amewakumbusha wananchi wa Arusha wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari, akisisitiza kuwa mapato hayo ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na chachu ya kuifanya Arusha kupiga hatua zaidi kiuchumi na kijamii.


Ziara hiyo pia ilijumuisha ukaguzi wa miradi mingine ikiwemo ujenzi wa Barabara ya ESO, mradi wa Soko la Kilombero pamoja na kukagua ujenzi wa jengo jipya la halmashauri linaloendelea kujengwa kwa kutumia mapato ya ndani ya jiji.








0/Post a Comment/Comments