Na
Bora Mustafa,
Arusha.
Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Daladala Wilaya ya Arusha, Musa Njuga, amesema anamshukuru Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, kwa uongozi wake wa kusikiliza wananchi na wadau wa sekta ya usafirishaji.
Njuga amesema kauli hiyo leo Aprili 25,2026 ameitoa baada ya kikao kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, ambapo walijadili changamoto zilizojitokeza hivi karibuni, ikiwemo tuhuma za baadhi ya madereva kupandisha nauli kiholela.
Pia Amesema kuwa madereva wanaelewa changamoto hizo na wako tayari kushirikiana na serikali kuhakikisha huduma ya usafiri inakuwa bora na yenye kuzingatia sheria.
Aidha, amesema operesheni iliyofanywa na Mkuu wa Wilaya ililenga kurejesha nidhamu katika sekta hiyo, ambapo baadhi ya magari na madereva walichukuliwa hatua ili kudhibiti ukiukwaji wa taratibu.
Hata hivyo Njuga amesema kupitia mazungumzo yaliyofanyika, madereva waliomba magari yaliyochukuliwa hatua yaruhusiwe kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya amekubali ombi hilo kwa kutoa msamaha, huku akisisitiza umuhimu wa madereva kuzingatia sheria, taratibu na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha Njuga amesema madereva wamejipanga kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya serikali ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza siku zijazo.

Post a Comment