CHAMPION D ATOA TABASAMU KWA WATOTO YATIMA WA KITUO CHA PARADISO ARUSHA


 

Na 

Bora Mustafa,

Arusha.

 Mdau wa michezo  Champion D, ametembelea Kituo cha Watoto Yatima cha Paradiso mpya kilichopo kata ya sinoni, mkoani Arusha, na kukabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo.

Akizungumza Leo Agosti 3,2026  baada ya kukabidhi msaada huo, Champion D amesema wazo la kuanzisha shughuli hiyo lilianza zaidi ya miaka mitatu iliyopita baada ya kuona watu kutoka maeneo mbalimbali nchini wakifanya matendo ya kusaidia jamii.

Aidha ameeleza kuwa safari ya kufanikisha wazo hilo haikuwa rahisi kutokana na changamoto mbalimbali za kupata wadau na maandalizi, lakini hakukata tamaa kwa kuwa aliamini dhamira yake ya kusaidia jamii ilikuwa ya muhimu.

Pia amewashukuru wadau wote waliomuunga mkono, wakiwemo watu wa sekta ya michezo, marafiki na mke wake ambaye amesema amekuwa nguzo muhimu katika kufanikisha shughuli hiyo.

Kwa upande wake, mmoja wa Mlezi wa Kituo cha Paradiso, Mama kaaya, amesema kituo hicho kilianza na watoto wanane na sasa kinahudumia watoto 27. Ameeleza kuwa licha ya kutokuwa na biashara au chanzo rasmi cha mapato, wameendelea kuhudumia watoto kwa neema ya Mungu na msaada wa wasamaria wema.

Aidha amesema watoto wengi waliokulia katika kituo hicho wamehitimu masomo yao, wengine wamepata ajira na bado wanaendelea kurudi kukitembelea kituo hicho.

Pia Mama kaaya ametoa shukrani kwa Champion D na wadau wake kwa msaada walioutoa, akisema umekuja wakati ambao kituo kilikuwa kinapitia kipindi kigumu.

Kwa upande wake Riziki Yusuf Bendera amesema kitendo kilichofanywa na Champion D kinapaswa kuwa mfano kwa vijana wengine na watu wote waliopo kwenye sekta ya michezo na vyombo vya habari, kwani kutoa sehemu ya walichonacho kwa jamii ni ishara ya uwajibikaji na upendo.

Hata hivyo ,  Mary Yohanes mwanafunzi wa kidato cha pili, ametoa shukrani kwa wote waliochangia msaada huo. Amesema kituo bado kinakabiliwa na changamoto za chakula, mavazi na ada za shule kwa baadhi ya watoto, huku akiwaombea wote waliowasaidia Mungu awabariki na awaongezee uwezo wa kuendelea kuwasaidia wenye uhitaji.



0/Post a Comment/Comments