Na
Bora Mustafa,
Arusha.
Katika juhudi za kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Ndugu John L. Kayombo, amekabidhi rasmi magari mawili mapya pamoja na mfumo wa matangazo (PA System) kwa watumishi wa jiji hilo.
Vifaa hivyo vimenunuliwa kwa kutumia mapato ya ndani ya jiji, hatua inayoonesha uwezo wa halmashauri kujitegemea kifedha huku ikiendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wake.
Mpango huo ni sehemu ya mikakati ya jiji katika kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa bora, za haraka na zenye ufanisi mkubwa.
Akizungumza Leo Aprili 28,2026 katika hafla hiyo, Mkurugenzi Kayombo amesema kuwa upatikanaji wa magari hayo pamoja na mfumo wa matangazo utasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kila siku.
Amesema shughuli zitakazonufaika ni pamoja na ukusanyaji wa mapato, ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na utoaji wa taarifa kwa umma kwa wakati.
Aidha, Kayombo amesema kuwa ni muhimu kwa watumishi waliokabidhiwa vifaa hivyo kuhakikisha wanavitunza kwa uangalifu na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija kwa jiji pamoja na wananchi .
Kwa upande wao, baadhi ya watumishi waliopokea vifaa hivyo wameishukuru menejimenti ya jiji kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi. Wamesema kuwa hatua hiyo itawasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Zoezi la makabidhiano limefanyika katika viwanja vya Jiji la Arusha, likihudhuriwa na watumishi mbalimbali pamoja na viongozi wa jiji hilo.



Post a Comment