Na
Mwandishi Wetu, Longido
Changamoto ya ukosefu wa chakula mashuleni imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wanafunzi wa shule za msingi Wilaya ya Longido mkoani Arusha, hali inayotajwa kuathiri mahudhurio na maendeleo yao ya kitaaluma.
Tatizo hilo limeelezwa kuwakumba zaidi wanafunzi wa MEMKWA, huku wadau wa elimu wakisema kuna haja ya juhudi za pamoja ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Akizungumza katika kikao cha Jukwaa la Wadau wa Elimu Leo mei 16,2026 kilichoandaliwa na Shirika la Utafiti, Maendeleo na Huduma za Jamii (CORDS), Afisa Elimu wa Kata ya Ngarenaibo, Paulo Teveli amesema wazazi wengi bado hawapeleki chakula shuleni jambo ambalo linaathiri wanafunzi wengi.
Pia Amesema baadhi ya wazazi hawajatoa umuhimu wa kutosha kwa elimu, huku wengine wakikabiliwa na changamoto za kiuchumi zinazowafanya kushindwa kuchangia chakula kwa watoto wao.
“Tatizo hili ni kubwa na linaathiri hata wanafunzi wa MEMKWA waliopo katika kata yetu. Tunahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kuhakikisha watoto hawa wanapata mazingira bora ya kusoma,” amesema Teveli.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Longido, Sein Kitomali amesema wanafunzi wengi hutoka umbali mrefu kufika shule, hivyo ukosefu wa chakula huathiri uwezo wao wa kujifunza darasani.
Amesema shule hiyo ina wanafunzi 62 wa MEMKWA, ambapo wanafunzi 38 wanatarajiwa kufanya mtihani wa darasa la nne mwaka huu.
Pia amesema msaada unaotolewa na shirika la CORDS umechangia kuwasaidia wanafunzi hao kupata vifaa muhimu vya kujifunzia na kuongeza hamasa ya kuendelea na masomo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngoswaki, Karia Mollel amesema jamii za wafugaji bado zinakabiliwa na changamoto ya kutothamini elimu, ingawa juhudi zinaendelea kufanywa kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto shule.
Hata hivyo Amesema viongozi wa vijiji wanaendelea kuwachukulia hatua wazazi wanaowazuia watoto kwenda shule sambamba na kuhamasisha uchangiaji wa chakula mashuleni.
Kwa upande wake, Meneja wa Elimu wa Shirika la CORDS, Ezekiel Piniel amesema jukwaa hilo limefanyika kupitia mradi wa Kupambana na Umasikini Kupitia Elimu na Uwezeshaji wa Kiuchumi (BELIEF), unaofadhiliwa na Shirika la Stromme Foundation.
Amesema mradi huo unalenga kusaidia wanafunzi, vijana pamoja na vikundi vya wajasiriamali katika wilaya za Longido na Ngorongoro.
Pia amesema kupitia mradi huo, shule za Ngoswaki na Longido zimekuwa zikisaidiwa vifaa vya kujifunzia, uboreshaji wa mazingira ya shule pamoja na kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Tunawasaidia pia vijana kupata stadi mbalimbali za maisha kupitia programu ya Bonga, huku vikundi vya wajasiriamali vikijengewa uwezo wa kutunza kumbukumbu, kusimamia miradi na kuhifadhi fedha,” amesema Piniel.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Longido, Nestory Dagharo amesema uchangiaji wa chakula mashuleni ni jambo la lazima katika wilaya hiyo kwani chakula hicho ndicho ambacho watoto wangekula nyumbani.
Amesema halmashauri inaendelea kufanya vizuri katika uandikishaji wa wanafunzi na kudhibiti utoro pamoja na ndoa za utotoni.




Post a Comment