Tawiri Yarejesha Matumaini kwa wananchi Kwa Kudhibiti Tembo Kisayansi .




Na 

Bora Mustafa,

Meatu .

Wananchi wanaoishi katika maeneo yenye migongano kati ya binadamu na tembo wameendelea kupata nafuu baada ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kuanza kutumia teknolojia ya kisasa ya kufunga mikanda yenye visukuma mawimbi (GPS) kwa tembo viongozi ili kudhibiti uvamizi wa wanyama hao katika makazi na mashamba ya wananchi.

Kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ikiwemo mabomu baridi pamoja na njia nyingine za jadi kukabiliana na tembo wanaovamia maeneo yao. Hata hivyo, hatua hiyo mpya ya kisayansi imeelezwa kuwa suluhisho la kudumu katika kupunguza migongano hiyo.

Akizingumza Leo Mei ,16,2026 Mtafiti na Daktari wa Wanyamapori kutoka TAWIRI, Dkt. Iddi Lipende, amesema mikanda hiyo ya GPS itakuwa ikitoa taarifa za mwenendo wa tembo muda wote. Amesema taarifa hizo zitasaidia askari wa vituo vya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu (PAC) kupata tahadhari mapema pindi tembo wanapoelekea kwenye makazi au mashamba ya wananchi.

Pia amesema mfumo huo utawezesha askari kuwazuia tembo hao kabla hawajasababisha madhara kwa wananchi na mazao yao.

Aidha, Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Meatu, Bw. Joseph Sikawa, amesema wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya uvamizi wa tembo mashambani kwa muda mrefu. Amesema vijiji vya Mwanyahina, Mwajidalala, Mwanzagamba, Mbugayabanya, Mwamashimba, Mang’wina, Mwangudo, Mbushi, Shushumi, Mbuyuni, Sungu pamoja na Paji ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi.

Pia Sikawa amesema serikali imeonyesha dhamira ya kweli ya kutatua changamoto hiyo kwa kuiwezesha TAWIRI kutekeleza mradi huo wa teknolojia ya GPS wilayani humo.

Kwa upande wake, mwananchi wa Wilaya ya Meatu, Godfrey Mabula, amesema hapo awali wananchi walilazimika kulala mashambani usiku kucha wakilinda mazao yao dhidi ya tembo.

 Amesema hali hiyo ilikuwa ikiwasababishia hofu pamoja na usumbufu mkubwa.

Pamoja na hayo, Mabula amesema matumizi ya teknolojia hiyo yatawasaidia wananchi kupata taarifa mapema kuhusu mienendo ya tembo na hivyo kupunguza hasara inayotokana na uvamizi wa wanyama hao.

Naye Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza kutoka TAWA, Bw. Ayubu Fundi, amesema askari uhifadhi wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuwarudisha tembo hifadhini, lakini wakati mwingine wamekuwa wakichelewa kuwafikia kutokana na wanyama hao kutokea maeneo mbalimbali ya hifadhi.

Amesema matumizi ya vifaa hivyo vya kisasa yataongeza kasi ya udhibiti wa tembo pamoja na kusaidia kupunguza migongano kati ya wananchi na wanyamapori.

Hatua hiyo inaendelea kuonyesha namna sayansi na teknolojia zinavyokuwa uti wa mgongo katika utafiti, uhifadhi endelevu pamoja na ulinzi wa maisha na mali za wananchi.





0/Post a Comment/Comments