Na
Mwandishi wetu, Lidya Lazaro
Monduli.
Mwanamke anaweza. Kauli hii imeendelea kudhihirika nchini Tanzania kupitia uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi na kuonyesha kuwa mwanamke akipewa nafasi anaweza kuleta mageuzi makubwa ya maendeleo.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Wilaya ya Monduli imebahatika kuongozwa na mwanamke jasiri, mwenye maono na mpenda maendeleo, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Gloriana Kimath. Tangu kuapishwa kwake kuiongoza wilaya hiyo, ameendelea kudhihirisha kwa vitendo kuwa uongozi si suala la jinsia, bali ni dhamira, uwajibikaji na kujitoa kwa ajili ya wananchi.
Aidha Wilaya ya Monduli ni miongoni mwa wilaya zenye utajiri mkubwa wa mila na desturi za jamii ya Kimasai, ambapo shughuli kuu za wananchi wake ni ufugaji na kilimo. Kutokana na upekee huo, Mhe. Gloriana Kimath ameendelea kuwa karibu na wananchi wa kada mbalimbali, akisikiliza changamoto zao na kushirikiana nao katika kutafuta suluhisho linalolenga kuinua uchumi na kuboresha ustawi wa jamii.
Leo, Juni 23, 2026, ikiwa ni mwaka mmoja tangu aanze rasmi majukumu yake Monduli, wananchi wanashuhudia matokeo ya uongozi wake wa karibu, wa kusikiliza na wenye kugusa maisha ya watu moja kwa moja. Katika kipindi hicho, amekuwa mstari wa mbele katika kutatua migogoro mbalimbali ya wananchi katika kata na vijiji tofauti vya wilaya hiyo. Kupitia usikivu wake, uvumilivu na busara za kiuongozi, migogoro mingi imepatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo na maridhiano, hali iliyosaidia kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Katika sekta ya elimu, Mhe. Gloriana Kimath ameendelea kuonyesha dhamira ya dhati katika kuhakikisha watoto wa Monduli wanapata elimu bora. Kupitia ziara zake za mara kwa mara shuleni, amekuwa akifuatilia maendeleo ya taaluma, kuhamasisha mahudhurio ya wanafunzi na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. Juhudi hizo zimeendelea kuongeza ari kwa walimu, wanafunzi na wazazi sambamba na kuimarisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu wilayani humo.
Pia Sekta ya afya nayo imeendelea kunufaika na uongozi wake. Amekuwa mstari wa mbele kufuatilia utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa kutembelea zahanati, vituo vya afya na hospitali mbalimbali, huku akisimamia utekelezaji wa miradi ya afya na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Katika sekta ya utalii, akiiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour, Mhe. Gloriana Kimath ameendelea kutangaza na kuhamasisha utalii ndani ya Wilaya ya Monduli. Amefanya ziara katika maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii ikiwemo Randilen Wildlife Management Area na Manyara Ranch Conservancy, kwa lengo la kujionea maendeleo ya sekta hiyo na kuhakikisha watalii wanaotembelea maeneo hayo wanapata huduma bora na kufurahia vivutio vya kipekee vinavyopatikana Monduli. Hatua hiyo imeendelea kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na kuongeza fursa za ajira kupitia sekta ya utalii.
Tofauti na viongozi wengi wanaobaki ofisini, Mhe. Gloriana Kimath amejijengea sifa ya kuwa kiongozi wa watu. Amefika vijijini, amesikiliza kero za wananchi moja kwa moja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo. Ukaribu huo umemfanya kuwa kiongozi anayependwa na kuheshimika na wananchi wa Monduli.
Kwa hakika, mwaka mmoja wa Mhe. Gloriana Kimath Monduli si mwaka wa maneno bali ni mwaka wa matokeo. Ni mwaka uliodhihirisha kuwa mwanamke akipewa nafasi anaweza kuongoza, kuunganisha jamii na kusimamia maendeleo kwa ufanisi.





Post a Comment