Wanafunzi ATC Wagundua Mfumo wa Kupiga Kura Kidijitali, Watakiwa Kusoma Dira ya Taifa 2050



Na Bora Mustafa, Arusha

Wanafunzi wanaojihusisha na ubunifu wa teknolojia mbalimbali katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) wametakiwa kuisoma na kuielewa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kutambua fursa zilizopo na kuzielekeza bunifu zao katika kutimiza malengo ya maendeleo ya taifa.

Akifungua Wiki ya Maonyesho ya Ubunifu inayofanyika kila mwaka chuoni hapo Juni 19, 2026, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Profesa Musa Chacha, amesema Dira ya Taifa 2050 imeainisha maeneo muhimu yanayopaswa kuendelezwa kwa ajili ya ustawi wa Watanzania, hivyo ni muhimu kwa wanafunzi kuyafahamu na kuyatumia kama msingi wa ubunifu wao.

Profesa Chacha amesema kutokana na kiwango kikubwa cha ubunifu kinachoendelea kuonyeshwa na wanafunzi wa chuo hicho, uongozi wa ATC umepanga kujenga jengo maalumu la ghorofa nne litakalotumika kwa shughuli za ubunifu na maendeleo ya teknolojia.

“Kwa kushirikiana na Serikali ya Italia, hivi karibuni tunatarajia kujenga jengo kubwa la ghorofa nne ambalo litatumika kwa shughuli za ubunifu (Innovation). Hapa chuoni hatutaki vipaji vyenu vipotee,” amesema Profesa Chacha.

Aidha, amesema chuo kinaendelea na ujenzi wa karakana ya viwanda (Industrial Workshop) ambayo itatumika kutengeneza mitambo bunifu inayogunduliwa na wanafunzi kwa lengo la kuizalisha na kuiingiza sokoni. Amesema mashine zitakazotumika katika karakana hiyo tayari ziko njiani kuwasili chuoni hapo.

“Hivi sasa tumeamua kuendeleza bunifu zote zitakazobuniwa na wanafunzi kwa kuzizalisha na kuziingiza sokoni. Tutakuwa na kiwanda hapa hapa chuoni, na wote mnaofanya ugunduzi huu tutaendelea kuwafuatilia ili kuona namna mnavyoweza kunufaika na bunifu zenu. Tutawashika mkono popote mtakapokwenda,” amesema profesa chacha.

Pamoja na hayo, Profesa Chacha amesema chuo kinakamilisha ujenzi wa hospitali itakayotoa huduma kwa wanafunzi. Aidha, kipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kujenga kituo maalumu cha ubunifu kitakachojulikana kama Innovation Center, ambacho kitahusika na ugunduzi na uzalishaji wa vifaa tiba kupitia taaluma ya Biomedical Engineering.

Amesema katika mashindano hayo jumla ya bunifu mbalimbali ziliwasilishwa kutoka katika fani tofauti, ambapo bunifu 20 zilikuwa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), 15 za umeme, 19 za mitambo na magari, nane za sayansi timizi na 13 za ujenzi pamoja na barabara. Hata hivyo, baada ya majaji kuzifanyia tathmini, bunifu 19 pekee ndizo zilizofanikiwa kuingia hatua ya fainali.

Profesa Chacha amesema mshindi wa kwanza ametoka katika fani ya mitambo baada ya kugundua mashine inayojulikana kama Energy Trauma Kit.

 Nafasi ya pili imechukuliwa na mbunifu kutoka TEHAMA aliyegundua mfumo wa kupima uwezo wa kuona wa macho unaojulikana kama VR Acute Test.

Aidha, amesema maonyesho hayo yana umuhimu mkubwa kwa taifa kwa kuwa yanawapa wanafunzi fursa ya kuonesha kwa vitendo maarifa wanayopata darasani, jambo linalochochea ukuaji wa ujuzi na ubunifu.

Katika baadhi ya bunifu zilizowasilishwa, Profesa Chacha amesema kulikuwa na wanafunzi waliobuni mfumo wa kupiga kura kwa njia ya kidijitali ambao unaweza kumwezesha mwananchi kupiga kura akiwa nyumbani.

“Katika bunifu hizi kuna vijana wametengeneza mfumo wa kupiga kura wakati wa uchaguzi ukiwa nyumbani. Teknolojia hii ikiendelezwa na kuboreshwa inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya uchaguzi nchini,” amesema.

Amesisitiza kuwa matarajio ya chuo ni kuona bunifu hizo zikifika kwa jamii na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili, huku ATC ikiendelea kuwekeza katika kukuza na kuendeleza vipaji vya wanafunzi wake.



0/Post a Comment/Comments