SHIRIKA LA HAND IN HAND LAUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KATIKA ELIMU.




Na

Egidia vedasto ,

Arusha.

Shirika la Hand in Hand limeunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha elimu kwa kusaidia upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA kwa wanafunzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

Akizungumza Leo Agost 08,2026 Mdau wa maendeleo kutoka shirika  hilo Noel Mgaya amesema shirika limekuwa mdau muhimu wa maendeleo ya elimu kwa kutoa kompyuta mpakato 105 kwa shule tano za sekondari zilizopo katika halmashauri hiyo.

Amesema lengo la msaada huo ni kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kukabiliana na mahitaji ya dunia ya kisasa.

Hatua hiyo pia inaelezwa kuwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza pamoja na vifaa vinavyowawezesha kupata maarifa na ujuzi unaohitajika.

pia Mgaya amesema, kupitia kompyuta hizo, wanafunzi pia wanatarajiwa kujifunza masuala ya usimamizi wa fedha, ujasiriamali,na mabadiliko ya tabia ya nchi jambo litakalowasaidia kukuza uwezo wa kujitegemea na kutumia maarifa wanayopata shuleni katika shughuli za kiuchumi.

Ushirikiano kati ya Shirika la Hand in Hand na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha unatarajiwa kuendelea kuwa mfano wa namna wadau mbalimbali wanavyoweza kushirikiana na Serikali katika kuimarisha elimu na kuandaa vijana wenye ujuzi wa TEHAMA, fedha na ujasiriamali.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Arusha Suleiman Msumi akimkabidhi cheti hicho Noel Mgaya amesema halmashauri inatambua mchango wa Shirika la Hand in Hand katika kuboresha elimu.

"Kipekee nawashukuru na kuwapongeza Kwa namna mmeichagua halmashauri yetu na kuwawezesha wanafunzi vifaa vya TEHAMA, nawaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yenu" amesema Msumi.


0/Post a Comment/Comments