KAFULILA: UBIA WA UMMA NA BINAFSI CHACHU YA KUONGEZA UFANISI NA AJIRA KWA VIJANA. Na


 

Na

Egidia Vedasto ,

Arusha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi David Kafulila amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya muda mrefu kwa lengo la kuongeza ufanisi na matokeo ya maendeleo.

Akizungumza Leo Septemba, 29,2026 Jijini Arusha amesema lengo la ubia huo ni kuvutia mtaji kutoka sekta binafsi, kutumia ubunifu uliopo katika sekta binafsi ambao wakati mwingine haupo serikalini, pamoja na kuongeza ufanisi wa kimenejimenti katika uendeshaji wa miradi na taasisi za umma.

Aidha amesema kuwa sekta za umma na sekta binafsi zina changamoto na mafanikio katika utekelezaji wa miradi, hivyo mkutano huo  unatoa fursa ya kujadili changamoto hizo na kutafuta majawabu yatakayosaidia kuongeza ufanisi.

 Kafulila ametoa mfano kuwa Tanzania inaweza kujifunza kutoka nchi za Kenya, Rwanda, India na Afrika Kusini ambazo, kwa mujibu wake, zimewaamini vijana na kuwapatia nafasi za ajira na uongozi, hatua inayosaidia katika kuongeza ufanisi na utekelezaji wa dira za maendeleo

Pia amepongeza na kuunga mkono kauli ya Makamu wa Rais, Deogratias Ndejembi, aliyoitoa wakati akihutubia  washiriki wa mkutano uliowahusisha wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi za umma na Binafsi nchini uliofanyika Jijini Arusha, ambapo ameyataka mashirika ya umma kutoa ajira Kwa vijana 10000 vivyo hivyo na Kwa mashirika binafsi.

"Kipekee nampongeza Makamu wa Rais Doegratias Ndejembi kuteuliwa kwake, naiona Tanzania katika mabadiliko chanya Kwa siku za usoni, matarajio ni  makubwa  yatawagusa vijana na taifa Kwa ujumla" amesema Kafulila.

Vilevile amebainisha kuwa muundo uliopo katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma una changamoto kwa kuwa Serikali ndiyo yenye jukumu la kuweka sera na kusimamia mashirika hayo, hivyo kuna umuhimu wa kuboresha mifumo ili kuongeza ufanisi na kuepuka hasara zisizo za lazima.

Aidha Kafulila amesema kuhusu fedha za kuwawezesha vijana kuhusu ajira, ameshauri badala ya vikao vya bodi za Mashirika ya Umma kufanyika nje ya nchi, vifanyike ndani ili fedha zinazotumika ziendelee kubaki nchini na kusaidia shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo kuwalipa vijana wanaoajiriwa.


0/Post a Comment/Comments