MICHEZO YA VIJANA: WADAU WATAKIWA KUKUZA VIPAJI, KUZINGATIA UMRI NA KUJENGA AMANI



 

Na 
Gladness kowero,
Arusha.

Mkurugenzi na mmiliki wa Trust St. Patrick Schools, Madam Dinna, amesema michezo ni ajira na chombo muhimu cha kuimarisha amani pamoja na kuwajengea vijana fursa za maisha, akiwataka wadau kuongeza juhudi katika kuibua na kukuza vipaji vya watoto tangu wakiwa katika umri mdogo.

Akizungumza  jana septemba 12,2026 baada ya kushuhudia bonanza la michezo lililofanyika katika shule ya St. Patrick jijini Arusha, lililoshirikisha akademi tano za michezo kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Arusha na Moshi kwa watoto wenye umri chini ya miaka 12, amesema ameridhishwa na namna vijana walivyoshiriki kwa furaha, nidhamu na kuzingatia kanuni za mchezo pamoja na maelekezo ya makocha wao.

Amesema michezo ina nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye amani, huku Tanzania ikiwa inajulikana kwa amani yake, hivyo ni muhimu fursa hiyo kutumika kuwajenga vijana na kuwaandaa kwa maisha pamoja na kuwapa nafasi ya kutumia vipaji vyao kama ajira hapo baadaye.

“Michezo ni ajira, lakini pia kila mahali ambako kuna michezo, amani hupatikana. Tanzania inapata sifa kubwa kwa amani yake, hivyo ni muhimu kutumia michezo kuendeleza amani na kuwajengea vijana fursa,” amesema Madam Dinna.

Kwa upande wa mgeni kutoka Denmark, Matthias, amesema amefurahishwa na fursa ya kushuhudia bonanza hilo, akivutiwa na furaha ya watoto pamoja na vipaji walivyoonyesha. Amesema uzoefu huo ni tofauti na mazingira anayoyafahamu nchini Denmark na amewataka watoto wenye vipaji kuendelea kuota, kujiamini na kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza ndoto zao.

Pia kwa upande wa mwanafunzi Mary Mremi ambae pia ni Mchezaji amewashauri vijana wanaotamani kufanikiwa katika soka kuondoa hofu, kujiamini na kuendelea kucheza mpira kwa bidii ili waweze kufikia malengo yao.

Pia amesema vijana hawapaswi kukata tamaa wanapokutana na changamoto, akieleza kuwa wakati wa kuanza kucheza mpira alikumbana na watu waliomkatisha tamaa na kumwambia asiendelee na mchezo huo.

Amesema licha ya changamoto hizo, hakukata tamaa, bali aliendelea kuamini katika uwezo wake na kuendelea kucheza, jambo ambalo limemsaidia kufikia hatua aliyopo sasa.

0/Post a Comment/Comments