Na
Egidia Vedasto
Arusha.
Mkurugenzi wa Shirika la ASPA, linalojihusisha na ustawi na ulinzi wa punda, Livingstone Masija, ameiomba Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka mikakati na sheria kali za kuhakikisha biashara haramu ya punda inakomeshwa nchini.
Akitoa mafunzo kwa Waandishi wa habari Jijini Arusha amesema punda ni mnyama muhimu katika jamii na kitega uchumi kinachookoa muda na gharama, huku akibainisha kuwa husaidia zaidi wanawake na watoto katika kubeba mizigo mbalimbali ikiwemo maji, kuni, mkaa na mazao.
Amesema katika baadhi ya mataifa yanayofanya biashara ya punda hasahasa China kumekuwa na dhana potofu kwamba bidhaa zitokanazo na mnyama huyo, ikiwemo ngozi, hutumika kutengeneza dawa za asili za kurefusha maisha pamoja na vipodozi, hali inayochangia kuongezeka kwa mahitaji ya punda.
Aidha, amesema punda wamekuwa wakisafirishwa kupitia njia zisizo rasmi, jambo ambalo limekuwa likisababisha ugumu katika kupambana na kudhibiti vitendo vya biashara hiyo haramu.
Ameongeza kuwa ASPA imekuwa ikilinda wanyama ambao hawapewi kipaumbele katika jamii, wakiwemo mbwa, paka na punda, ambao mara nyingi hawapati chanjo, malisho bora wala mazingira mazuri ya malazi.
Amesema baada ya Serikali kufunga viwanda vya Wachina vilivyokuwa vikifanya biashara ya punda katika mikoa ya Dodoma na Geita, ulinzi wa punda umeimarika, ingawa bado vimeripotiwa baadhi ya vitendo vya utoroshaji wa wanyama hao.
Katika hatua nyingine, Masija amewataka waandishi wa habari kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa punda kama mnyama wa kazi na chanzo cha kipato, huku akiiomba Serikali kumtambua na kumlinda mnyama huyo kwa umuhimu unaostahili, kama ilivyo kwa wanyama wengine.
Kwa upande wake Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la Habari Tanzania Grace Macha amesema mafunzo hayo yamewasaidia waandishi wa habari kujengewa uwezo kuhusu namna ya kuelimisha jamii juu ya umuhimu na matunzo sahihi ya mnyama punda.
Amesema kupitia mafunzo hayo, waandishi wamepata uelewa zaidi kuhusu changamoto zinazowakabili punda pamoja na umuhimu wa kuhakikisha wanapatiwa matunzo bora, ikiwemo chakula, maji, matibabu na mazingira salama ya kuishi.
Ameongeza kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii na kuendelea kupiga vita biashara haramu ya punda, huku akiwataka kutumia vyombo vyao vya habari kufikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa kumlinda na kumtunza mnyama huyo.
Daktari wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Robert Buluba, amewataka wafanyabiashara na wafugaji kufuata sheria na taratibu za usafirishaji wa mifugo ndani na nje ya nchi ili kuepuka kadhia wanazoweza kukumbana nazo.
Amesema ni muhimu wafanyabiashara na wafugaji kuhakikisha wanazingatia matakwa ya kisheria wakati wa kusafirisha wanyama, ili kuepusha vitendo vya usafirishaji usio halali pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa na mamlaka husika.
Dkt.Buluba amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha mnyama punda anatambuliwa na kulindwa kama ilivyo kwa wanyama wengine, kwa kuzingatia Sheria ya Ustawi wa Wanyama na matakwa ya Katiba ya nchi.


Post a Comment