BRELA YATOA ELIMU KWA WASANII KUHUSI USAJILI NA ULINZI WA ALAMA ZA BIASHARA.



 

Na,

 Egidia Vedasto,

 Arusha.

Wasanii walioshiriki maonyesho ya utalii wa Sanaa yanayofanyika katika viwanja wa General tyre Njiro Arusha wamepata ufafanuzi wa namna ya kusajili biashara zao na jinsi ya kuzilinda.

Akizungumza jana octoba 08 ,2026 Msaidizi wa usajili mkuu,kurugenzi miliki bunifu wa BRELA Nassoro Mtavu amewapa majibu na kusema kuwa mtu hawezi kufungua kiwanda au kuanzisha biashara bila kuisajili BRELA, ikiwa ni pamoja na kupata jina au alama ya biashara hiyo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Aidha amesema usajili huo humsaidia mfanyabiashara kujitofautisha na wafanyabiashara wengine, kulinda utambulisho wa biashara yake na kuhakikisha anakuwa na upekee katika soko.

Awali akijibu maswali ya wasanii katika warsha Mtavu ameeleza kuwa logo, nembo au alama ya biashara (trademark) husajiliwa katika madaraja mbalimbali kulingana na aina ya bidhaa au huduma ambayo mmiliki anataka kuilinda. Hivyo, usajili wa alama hauhusishi moja kwa moja bidhaa zote, bali unategemea daraja ambalo bidhaa husika imeainishwa.

Pia amesema kuna madaraja 45 ya bidhaa na huduma, ambapo kila daraja lina bidhaa zake. Kwa mfano, Daraja la 25 linahusisha bidhaa kama nguo, viatu, kofia na mikanda, wakati Daraja la 4 linahusisha bidhaa za manukato. Aidha, Daraja la 30 linahusisha bidhaa za chakula.

Mtavu mesema" Endapo mtu anataka kusajili na kulinda alama yake kwa ajili ya bidhaa za chakula, anatakiwa kuomba usajili katika daraja linalohusisha bidhaa hizo. Usajili huo hautampa ulinzi wa moja kwa moja katika bidhaa zilizo kwenye madaraja mengine"

Amefafanua kuwa sababu ya utaratibu huo ni kwamba kila daraja limeainishwa kulingana na aina maalumu ya bidhaa au huduma. Kwa hiyo, mmiliki wa alama anayefanya biashara katika zaidi ya kundi moja la bidhaa anapaswa kuzingatia madaraja husika ili kuhakikisha alama yake inalindwa kwenye bidhaa zote anazozalisha au kuuza.

" Bidhaa za vinywaji na bidhaa nyingine zinaweza kuwa katika madaraja tofauti, hivyo haiwezekani kudhani kwamba kusajili alama katika daraja moja kunamaanisha imelindwa moja kwa moja katika madaraja mengine" amesema Mtavu.




Hata hivyo, amewashauri wasanii na wafanyabiashara wanaotaka kulinda logo, nembo au alama zao kuhakikisha wanafahamu bidhaa au huduma wanazofanyia biashara na madaraja yanayohusika kabla ya kufanya usajili, ili kupata ulinzi unaoendana na shughuli zao.

Kwa upande wake Zainab Zayumba mfanya biashara ya Vinyago, ametaka kufahamu juu ya kusajili jina Moja Kwa bidhaa tofauti, amewashukuru BRELA Kwa kumpa mwanga na majibu ya maswali aliyokuwa nayo Kwa muda mrefu.

Pia amewaomba BRELA kuendelea kutoa elimu mara Kwa mara Kwa wafanyabiashara wakiwemo wasanii kwani hawana elimu ya kutosha hatua inayopelekea kuishia kuwalaumu.

0/Post a Comment/Comments