Na,
Egidia Vedasto,
Arusha.
Msaidizi wa usajili mkuu, Mkurugenzi miliki bunifu kutoka BRELA Nassoro Mtavu wakati akizungumza na wadau wa sanaa katika maonyesho ya Arusha Artisan Festival yanayoendelea katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha, amesema yeye na timu yake wamejiandaa kuwasaidia wasanii kurasimisha biashara zao.
Amesema hayo leo octoba 07,2026 wakati wa tamasha la Arusha Artisan Festival amesema Brela inalenga kuwawezesha wasanii kufanya shughuli zao kwa utaratibu unaotambulika kisheria na kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa kwa wafanyabiashara waliosajiliwa.
Aidha Mtavu amesema wasanii wana nafasi ya kupata ufafanuzi kuhusu taratibu za usajili wa biashara pamoja na masuala mengine yanayohusiana na shughuli zao kupitia wataalamu waliopo katika maonyesho hayo.
Amesema "Maonyesho hayo yamekuwa fursa muhimu kwa wasanii na wafanyabiashara kupata elimu kuhusu namna ya kuendesha na kukuza shughuli zao kwa kuzingatia taratibu za kisheria,
wadau wa sanaa tumieni nafasi hii kuuliza maswali kuhusu changamoto zinazowakabili katika shughuli zenu za kila siku".
Amesema wasanii wanapaswa kuibua changamoto zinazowatatiza ili kupata majibu na ufumbuzi unaofaa kutoka kwa wataalamu wa masuala ya biashara na usajili, alama za biashara, majina ya biashara na mambo mengine.
Vilevile Mtavu amewahimiza wasanii kutumia fursa hiyo kupata elimu kuhusu shughuli za BRELA na masuala yanayowahusu wafanyabiashara, akisema elimu hiyo itawasaidia kurasimisha biashara zao na kuzikuza kwa ufanisi.

Post a Comment