ATC YAWAANDAA WAHITIMU KUKABILI SOKO LA AJIRA KWA UJUZI WA VITENDO.





Na

Egidia Vedasto, 

Arusha.

Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kimeendelea kuimarisha mifumo yake ya ufundishaji kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia duniani, kwa lengo la kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi na uwezo wa kushindana katika soko la ajira.

Kuanzishwa kwa Kiwanda cha Ujifunzaji (Teaching Factory) chuoni hapo kunalenga kuwawezesha wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo, kukuza ubunifu na kuimarisha uwezo wao wa kutumia teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi, hatua inayotarajiwa kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Akizungumza katika mahafali ya 18 ya chuo hicho, yaliyohusisha wahitimu 1,337 kutoka programu mbalimbali za mafunzo katika ngazi tofauti, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Fredrick Salukele, ameielekeza Bodi ya Menejimenti ya chuo hicho kuandaa mpango madhubuti wa uendeshaji wa Kiwanda cha Ujifunzaji ili kuhakikisha kinaleta mageuzi chanya katika mafunzo ya ufundi.

Aidha, ameitaka menejimenti ya chuo hicho kuimarisha ubora wa mitaala na mifumo ya tathmini ya umahiri kwa kushirikiana na waajiri, kuhamasisha wanawake kujiunga na fani za sayansi na uhandisi pamoja na kuweka mifumo imara ya uwekezaji itakayokuwa na manufaa ya muda mrefu.

Ametoa mfano wa mradi wa uzalishaji umeme unaotekelezwa katika Chuo cha Ufundi Kikuletwa kilichopo Hai, mkoani Kilimanjaro, ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 1.6 za umeme zitakazonufaisha wilaya nzima.

"Nawapongeza kwa ubunifu wa kutengeneza mita za awali za malipo ya kabla, ambazo zitasaidia kukuza ujuzi wa kiufundi na kutoa fursa ya kutumia maarifa katika mazingira halisi. Watumieni vizuri wataalamu kutoka vyuo vikuu vya nje, ikiwemo Korea Kusini na nchi nyingine, ili kutusaidia kuimarisha ujuzi na kupunguza utegemezi," amesema.

Vilevile, amewahimiza wahitimu kuwa waaminifu, waadilifu, wazalendo na wabunifu, huku akiwataka kuendelea kujifunza na kuendana na mabadiliko ya teknolojia ili kukabiliana na ushindani katika soko la ajira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Ufundi Arusha, Profesa Mussa Chacha, amesema wahitimu wa chuo hicho ni kama madini ya Tanzanite kutokana na ujuzi na maarifa adimu wanayoyapata kupitia mafunzo ya vitendo wanayopitia chuoni hapo.

Ameiomba Serikali pamoja na wadau wa sekta binafsi kuwapa nafasi wahitimu hao katika maeneo yao ya kazi ili waweze kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata chuoni kutatua changamoto na kuchangia maendeleo ya taifa.

Profesa Chacha ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika ujenzi na uboreshaji wa karakana za kisasa chuoni hapo, akisema uwekezaji huo umeimarisha mazingira ya mafunzo na kuwaandaa vijana kuwa nguvu kazi yenye maarifa na ujuzi unaohitajika katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Amesema, "Kipekee nawapongeza watumishi kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuwafundisha vijana hawa. Weledi walioupata utawatofautisha na wengine katika soko la ajira. Niwaombe wahitimu wote, mtakapohitaji msaada msisite kurudi chuoni wakati wowote. Naw takia kila la heri katika maisha yenu."

Mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Kompyuta, Happyphania Ndolingo, amesema elimu aliyopata katika Chuo cha Ufundi Arusha imemjengea uwezo wa kujiajiri badala ya kutegemea ajira serikalini pekee.

Amesema wakati wa masomo yake alikuwa akijiwekea akiba kidogo kidogo, jambo ambalo limemwezesha kuwa na mtaji wa kuanzisha biashara ya duka la vifaa vya shule (stationery) huku akiendelea kusubiri fursa nyingine za ajira.


Kwa upande wake, Brighton Ngunguru, mhitimu wa Stashahada ya Uhandisi wa Ujenzi, amesema yuko tayari kukabiliana na ushindani wa soko la ajira kutokana na ujuzi alioupata kuhusu matumizi ya vifaa vya kisasa visivyochafua mazingira katika shughuli za ujenzi, akiamini maarifa hayo yatamwezesha kutoa huduma bora na kuwavutia wateja.



0/Post a Comment/Comments