CHITINKA ATOA WITO KWA WANACHAMA KUTUMIA FURSA ZA PCCB SACCOS.


 

Na,

Egidia Vedasto,

Arusha.

Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Dodoma Joseph Chitinka amesema chama cha ushirika ni chombo muhimu cha kujenga na kufanya maamuzi, kujadili mafanikio na changamoto pamoja na kupanga bajeti ya mwaka unaofuata 2027 kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya chama na wanachama wake.

Akizungumza Leo Novemba 16,2026 katika mkutano wa 23 wa mwaka wa PCCB SACCOS Jijini Arusha, amesema viongozi na wasimamizi wa chama hicho wanaendelea kuzingatia sheria, taratibu na miongozo mbalimbali inayosimamia uendeshaji wa chama ili kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya ushirika.

Aidha, Chitinka amesema kuwa Saccos ya PCCB Dodoma imeendelea kufanya vizuri na kushika nafasi ya 8 kati ya vyama  20 bora.

Ameongeza kuwa wataendelea kuwahamasisha watumishi kujiunga na chama hicho ili waweze kupata fursa za kifedha na huduma zinazotolewa na chama, badala ya kutegemea taasisi nyingine za kifedha zenye gharama kubwa na masharti yanayoweza kuwaathiri na kuwadhalilisha.

Chitinka amesisitiza kuwa chama ni mali ya wanachama wenyewe, hivyo wanapaswa kutumia fursa zilizopo ndani ya chama badala ya kukopa katika benki nyingine. 

Sambamba na hayo amewataka wanachama wanaokopa kuhakikisha wanarejesha mikopo yao kwa wakati ili kuwawezesha wanachama wengine kupata nafasi ya kukopa na kuendeleza shughuli zao.

Pia amewataka viongozi wengine wa chama kutendea kazi maagizo ya Mkurugenzi Mtendaji wa TAKUKURU na mlezi wa chama Crispin Chalamila kuhakikisha wanachama wanaongezeka.

 

0/Post a Comment/Comments