Na,
Egidia Vedasto,
Arusha.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, Dkt. Tibrus Makoi, ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira yaliyomwezesha kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari bingwa, akisema elimu aliyopata katika shule za Serikali pamoja na mkopo wa elimu ya juu vilikuwa chachu ya mafanikio yake.
Akizungumza jana novemba ,10,2026 Amesema tangu akiwa katika ngazi ya elimu ya msingi hadi chuo kikuu, alipata fursa ya kusoma katika shule za Serikali, huku mkopo wa elimu ya juu ukimsaidia kukamilisha masomo yake na kufikia ndoto ya kuwa daktari.
Dkt. Makoi ametoa pongezi kwa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kwa kutimiza miaka 100 tangu kuanza kutoa huduma za afya mwaka 1926, akieleza kuwa ni hatua muhimu inayoonesha mchango wa hospitali hiyo katika kuhudumia wananchi kwa kipindi cha karne moja.
Aidha, ameishukuru hospitali hiyo kwa kumtambua na kumpa cheti cha Daktari Bora na Mwenye Kujituma, akisema utambuzi huo ni chachu kwake kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Dkt. Makoi amesema safari yake ya kuitumikia hospitali hiyo ilianza kwa kujitolea kabla ya kupata ajira rasmi mwaka 2021, hatua iliyompa fursa ya kuendelea kutumia taaluma yake kuhudumia wananchi wanaofika hospitalini hapo kupata matibabu.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha utumishi wake, ambacho ni takribani miaka sita, amepata uzoefu mkubwa wa kitaaluma na kushuhudia mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa na hospitali hiyo katika kuboresha huduma za afya.
Amesema "Mount Meru imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya za kimsingi pamoja na huduma za kibingwa, jambo linalowezesha wagonjwa kupata huduma mbalimbali kulingana na mahitaji yao ya kiafya"
Dkt. Makoi ameongeza kuwa kutimiza miaka 100 kwa hospitali hiyo ni fursa ya kutambua mchango wa watumishi wote walioitumikia kwa miaka mingi, huku akiahidi kuendelea kujituma katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
.jpg)

Post a Comment