KAMATI YA MASUALA MTAMBUKA BUNGE LA A.MASHARIKI YAKAMILISHA UCHAMBUZI WA MUSWADA WA KUTOKOMEZA UKEKETAJI.


 

Na,

 Egidia Vedasto,

Arusha.

Kamati ya Masuala ya Jumla ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki imekamilisha kikao cha kupitia maoni ya nchi wanachama kuhusu Muswada wa Sheria ya Kutokomeza Ukeketaji wa Wanawake na Wasichana, unaolenga kukomesha vitendo hivyo katika ukanda huo.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Masuala Mtambuka ya Bunge hilo, Dr. Abdullah Hasnuu Makame amesema Bunge hilo linaandaa muswada wa sheria unaolenga kutokomeza vitendo vya ukeketaji wa wanawake na wasichana katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Amesema Kwa muda wa siku mbili, kamati imekuwa ikipitia muswada huo kipengele kwa kipengele ili kukamilisha uchakataji wake kabla ya kuuwasilisha katika kikao cha Bunge kinachotarajiwa kufanyika mapema Desemba mwaka huu.

Ameongeza kuwa muswada huo unaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na jamii, akieleza kuwa ukeketaji ni utamaduni usiofaa, unaokiuka haki za wanawake na kuwa na madhara makubwa kiafya, ikiwemo kupoteza damu nyingi, kuchanika na kupata matatizo wakati wa kujifungua, hali inayoweza kuhatarisha maisha yao.

Aidha, Dr. Makame amewataka wakuu wa nchi wanachama na wadau mbalimbali kuunga mkono na kuridhia muswada huo utakapopitishwa na Bunge ili uweze kutekelezwa katika ukanda huo.

"Kutokomeza ukeketaji ni kutenda haki kwa wanawake, jamii na ubinadamu kwa ujumla,  matumaini yangu ni kuwa juhudi hizo zitafanya vitendo hivyo kutoweka na kubaki historia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki" amesema Dr. Makame.

Kwa upande wake  Mjumbe wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Jamhuri ya Rwanda, Caroline Rwivanga Kayonga, amesema Kamati ya Masuala ya Jumla ya Bunge hilo imekamilisha kupitia maoni yaliyotolewa na nchi wanachama kuhusu Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kutokomeza Ukeketaji wa Wanawake na Wasichana (FGM).

Akizungumza kuhusu hatua iliyofikiwa katika muswada huo, Kayonga amesema kamati hiyo imetumia siku mbili kupitia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau kutoka nchi wanachama wakati wa mikutano ya mashauriano ya umma iliyofanyika kwa kipindi cha takribani miaka miwili.

Amesema mwaka 2025 mikutano hiyo ya mashauriano ilifanyika katika nchi sita wanachama ambazo ni Burundi, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda, Sudan Kusini na Tanzania, huku mwaka huu ikifanyika katika Jamhuri ya Shirikisho la Somalia.

Amesema kuingia kwa Somalia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kulifanya kuwe na umuhimu wa kufanya mashauriano ya umma nchini humo ili kupata maoni ya wadau wake na kuhakikisha muswada huo unazingatia mitazamo na mahitaji ya nchi zote wanachama.

"Kamati ilifanya kazi ya kupitia maoni hayo kipengele kwa kipengele, kuyajadili na kutathmini namna yanavyoweza kuingizwa katika muswada huo ili kuuboresha kabla ya kuwasilishwa katika hatua zinazofuata za kisheria",

"Mchakato huo ulikuwa na changamoto kutokana na wingi wa maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wadau na nchi wanachama, jambo lililohitaji muda na uchambuzi wa kina, lakini kamati imefanikiwa kuyapitia na kuyafanyia kazi" amesema.

Kayonga ameongeza kuwa kilichobaki ni kukamilisha ripoti ya kamati pamoja na kukutana na Mwandishi Mkuu wa Sheria ili kuandaa jedwali la marekebisho yatakayofanyika katika muswada huo.

Katika namna hiyo hiyo mjumbe wa kamati hiyo kutoka Jamhuri ya Rwanda Fatuma Ndangiza, amesema moja ya ajenda muhimu iliyojadiliwa ni Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kutokomeza Ukeketaji wa Wanawake na Wasichana, ambao unalenga kukomesha mila hiyo inayofanyika katika baadhi ya jamii za nchi wanachama.

Amesema katika kikao hicho kilichofanyika Kwa siku mbili  kamati iliwaalika wadau mbalimbali kujadili muswada huo na kupitia ripoti iliyokusanywa kutokana na maoni na michango ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ndangiza ameeleza kuwa katika kuandaa muswada huo, kamati ilitembelea nchi mbalimbali wanachama kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi na wadau ili kuhakikisha sheria inayopendekezwa inazingatia mazingira na mahitaji ya nchi hizo.

Sambamba na hayo amesema kuna matumaini kuwa katika kikao cha Bunge la Afrika Mashariki kinachotarajiwa kufanyika mapema  Desemba mwaka huu, muswada huo utajadiliwa na kupitishwa ili uweze kuwa sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Vile vile amesisitiza kuwa endapo muswada huo utapitishwa, utasaidia kuimarisha usawa wa kijinsia na kulinda haki za binadamu, hususan haki za wanawake na watoto wa kike, pamoja na kuweka msingi wa kukomesha vitendo vya ukeketaji katika nchi za Afrika Mashariki.

0/Post a Comment/Comments