Na,
Egidia Vedasto,
Arusha.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru imeadhimisha miaka 100 tangu ilipoanza kutoa huduma za afya 1926 na kuahidi kuendelea kutoa huduma za afya kidigitali na kufunga vifaa vya kisasa vya uchunguzi Kwa wakazi wa Arusha, mikoa na mataifa jirani.
Akizungumza Leo Novemba 10,2026 katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya hospitali hiyo, Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa amesema watangulizi wa huduma za afya walioweka misingi imara katika hospitali hiyo tangu vita ya kwanza ya dunia 1915 wataendelea kukumbukwa.
Amesema mwaka 1961 Tanzania ilikuwa na watu wasiozidi milioni 9, na Daktari 12 na leo hii nchi ina madaktari 12,600. Hatua inayodhihirisha mafanikio katika sekta ya afya.
Aidha ameipongeza serikali Kwa hatua kubwa ya mafanikio ya sekta ya afya kiasi cha kutegemewa na mataifa jirani. Amesema katika mafanikio hayo awamu zote za serikali zinatakiwa pongezi Kwa maono yake.
Amesema"Kipekee nawapongeza Watumishi wa hospitali hii mkiongozwa na Mganga mfawidhi wa hospitali hii, Kwa kutambua umuhimu huo Mganga mfawidhi hakikisha unawapa vyeti Kwa kutambua kazi yao nzuri wanayoifanya".
Mchengerwa amewahimiza Wananchi kupima na kufahamu hali za afya zao, amesisitiza kuanzisha Kambi za matibabu katika masoko, misikiti na makanisa bure Ili kuwasaidia Wananchi kutambua hali zao.
Vile vile amewataka viongozi wa mikoa na Wilaya kuendelea kuhamasisha kufanya mazoezi ya mara kwa mara Ili kupunguza magonjwa nyemelezi yasiyokuwa ya kuambukizwa.
Mchengerwa ameeleza "Serikali inaweza kununua MRI lakini haiwezi kuleta huruma, wakati serikali inaendelea kuleta tabasamu Kwa watu wake, Watumishi tendeni kazi Kwa huruma na kuacha alama ya upendo na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita Kwa kuwaachia tabasamu wananchi".
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Alex Ernest ameishukuru serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika hospitali hiyo na kuipa hadhi ya kuwa hospitali ya Rufaa inayoaminika kwa huduma bora ndani na nje ya nchi.
Amesema Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru inaendelea kupiga hatua mbele Kwa kasi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan Kwa kutoa tiba za Kansa, tiba za kemikali, uwezo wa Huduma za uchunguzi, tiba za oxygen, Kambi za matibabu na Huduma nyingine nyingi.
"Tunapoadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa Kwa Huduma za afya katika hospitali yetu 1926 kutoka kuwa kituo cha afya na kuwa hospitali ya Rufaa ya mkoa, tunapoianza Karne ya pili nawashukuru na kuwapongeza Watumishi wote wa hospitali hii na tunatazamia kuendelea kuwa wavumbuzi na kutoa huduma bora isiyokoma" amesema Dkt. Alex.
Kwa upande wake Katibu mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe amesema Ushirikiano ndio msingi mkuu wa Huduma za afya.
Amesema kuwa katika maadhimisho hayo ni vyema kuendelea kuwaenzi watangulizi na wastaafu kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa maono ambayo yameleta mafanikio na mageuzi makubwa.
Pamoja na hayo ameishukuru serikali Kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika Kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo wa sekta binafsi wanaounga mkono juhudi za serikali kupitia sekta ya afya.
"Sekta ya afya imeendelea kuboreshwa kila mahali, Huduma ya upandikizani viungo vyote unafanyika hapa, na upimaji wa utendaji wa utawala bora Tanzania imeshika nafasi ya 8 kati ya nchi 54 za Afrika na kushika nafasi ya kwanza Afrika Mashariki" amesema Dkt.Grace.
Vilevile Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge Afya na UKIMWI na Mbunge wa Mbulu vijijini Emmanuel Kambaji ameiomba serikali kuhakikisha inapambana kumaliza vifo vya mama na mtoto na wanaojifungulia nyumbani.
Pia Kambaji ameiomba serikali kufanya jitihada za maboresho ya miundombinu ya majengo ya hospitali hiyo. Sambamba na hayo ameahidi ushirikiano wa karibu na hospitali hiyo Ili kuhakikisha wanapitisha bajeti itakayoiwezesha kusonga mbele katika utoaji huduma za afya Kwa wazawa na Watalii.




Post a Comment