Na,
Egidia Vedasto,
Arusha.
Wananchama zaidi ya 600 wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo PCCB wamekutana kushiriki mkutano wao wa mwaka Jijini Arusha kujadili mafanikio, changamoto na mstakabali wa chama chao.
Akizungumza Leo Novemba 16,2026katika ufunguzi wa mkutano wa 23 wa mwaka wa chama cha Ushirika wa akiba na mikopo (PCCB SACCOS LTD) Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini, Crispin Cahalamila, ambaye pia ni mlezi wa Chama amewataka wanachama kutumia muda wa mkutano kujadiliana kwa tija na kuweka utaratibu mzuri wa kuhudhuria mikutano bila kuathiri majukumu yao kwa waajiri.
Amesisitiza umuhimu wa wanachama kupata elimu ya fedha, uwekezaji na bima ili kuwajengea uwezo wa kusimamia rasilimali zao, kuongeza kipato na kuzingatia nidhamu ya uwekezaji. Aidha, amewataka kuepuka madai yasiyo ya lazima yanayoweza kuathiri maendeleo yao na chama.
Chalamila amepongeza mafanikio yaliyopatikana na chama hicho, ikiwemo ongezeko la idadi ya wanachama, akiba na hisa, akieleza kuwa hatua hizo zinaonesha maendeleo katika uimarishaji wa chama na ustawi wa wanachama wake.
Pia amepongeza ajenda ya utoaji wa elimu ya bima, akisema itasaidia kulinda mali, maisha na kukuza mtaji wa wanachama.
Amewataka wanachama wanaokopa kuhakikisha wanarejesha mikopo yao kwa wakati ili kulinda mtaji wa chama na kuepusha changamoto zinazoweza kurudisha nyuma maendeleo yake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Ushirika PCCB, Betrod Busanda amesema ajenda muhimu zitakazojadiliwa ni pamoja na sera ya ushiriki na uendeshaji wa mikutano mikuu ya chama, taarifa maalumu kuhusu utafutaji wa kiwanja kwa ajili ya kujenga ofisi za chama na uwekezaji, makisio ya mapato na matumizi pamoja na utoaji wa elimu ya bima. Aidha, amesema chama kinalenga kuwezesha idadi toshelezi ya wanachama kushiriki katika mkutano huo.
Amesema katika kipindi cha uongozi wa bodi hiyo kumekuwa na mafanikio mbalimbali, likiwemo ongezeko la idadi ya wanachama kutoka 2,363 walioandikishwa Septemba 30, 2025 hadi kufikia wanachama 2,549 Septemba 30, 2026.
Busanda ameeleza kuwa akiba za wanachama pia zimeongezeka kutoka Sh Bilioni 25,817,727,176 Septemba 30, 2025 hadi Sh Bilioni 31,860,212,155, huku akitaja ongezeko la hisa za wanachama kuwa sehemu ya mafanikio yaliyopatikana.
Aidha, amesema chama kimefanikiwa kutoa mikopo kwa wanachama 5,522 kiasi shilingi Bil. 43,232,239,165. Ameongeza kuwa wanachama 21 wamekombolewa kutoka katika mikopo ya benki kupitia huduma ya “Nikomboe”.
Vilevile Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Dodoma Joseph Chitinka amesema chama cha ushirika ni chombo muhimu cha kujenga na kufanya maamuzi, kujadili mafanikio na changamoto pamoja na kupanga bajeti ya mwaka unaofuata kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya chama na wanachama wake.
Amesema viongozi na wasimamizi wa chama hicho wanaendelea kuzingatia sheria, taratibu na miongozo mbalimbali inayosimamia uendeshaji wa chama ili kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya ushirika.
Aidha, amesema wataendelea kuwahamasisha watumishi kujiunga na chama hicho ili waweze kupata fursa za kifedha na huduma zinazotolewa na chama, badala ya kutegemea taasisi nyingine za kifedha zenye gharama kubwa na masharti yanayoweza kuwaathiri.
Chitinka amesisitiza kuwa chama ni mali ya wanachama wenyewe, hivyo wanapaswa kutumia fursa zilizopo ndani ya chama badala ya kukopa katika benki nyingine.
Sambamba na hayo amewataka wanachama wanaokopa kuhakikisha wanarejesha mikopo yao kwa wakati ili kuwawezesha wanachama wengine kupata nafasi ya kukopa na kuendeleza shughuli zao.

Post a Comment