Na,
Egidia Vedasto, Arusha.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza S. Johari, amesema uzinduzi wa Kamati za Kudumu za Ushauri wa Kisheria katika ngazi za mikoa na wilaya pamoja na Kliniki ya Sheria bila malipo ni mwendelezo wa mikakati ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisheria kwa urahisi.
Amesema kupitia huduma hiyo, wananchi watapata fursa ya kusikilizwa na kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria, zikiwemo masuala ya kifamilia, migogoro ya ardhi na changamoto nyingine zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Akizindua kamati hizo pamoja na Kliniki ya Sheria bila malipo mkoani Arusha, Mheshimiwa Johari amesema utaratibu huo utasaidia kupunguza mzigo kwa Mahakama kwa kushughulikia changamoto zinazoweza kutatuliwa nje ya mfumo wa mashauri ya kimahakama.
Amewataka mawakili wa Serikali na wa kujitegemea kutoa huduma kwa wananchi kwa huruma, weledi na umahiri, akieleza kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya kutekeleza wajibu wao katika kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya 2050.
Aidha, amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa jirani kufika katika viwanja vya Sanawari kupata huduma za kisheria bila malipo, zitakazotolewa kwa muda wa siku tano.
Mheshimiwa Johari amesema kuwa kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi ni hatua muhimu katika kujenga taifa lenye maendeleo, akibainisha kuwa hadi sasa mpango huo umefika katika mikoa tisa na kuwahudumia wananchi 11,715 bila malipo.
Kuwasikiliza wananchi kuhusu changamoto zao na kuzipatia majibu ni mojawapo ya hatua za kujenga taifa lenye uhai. Tumefanikiwa kufikia mikoa tisa hadi sasa na kusikiliza wananchi 11,715 bila malipo," amesema Johari.
Kwa upande wake, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Alice Mtulo, ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa huduma hiyo bila malipo, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuwasaidia wananchi kupata haki na kutatua changamoto zao za kisheria.
Amesema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inatambua umuhimu wa majukumu ya kamati hizo, yakiwemo kusikiliza mashauri dhidi ya Serikali, kuokoa gharama za Serikali pamoja na muda unaotumika katika kushughulikia mashauri hayo.
"Utaratibu huu wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi utawapa muda wa kutosha wa kufanya shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi wao badala ya kutumia muda mwingi kutafuta haki mahakamani," amesema Mtulo.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Grace Kapama, amesema Mahakama inaungana na taasisi nyingine zilizoshiriki kufanikisha kliniki hiyo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata haki, amani na mazingira bora ya kujijenga kiuchumi.
Amewahimiza wananchi wa Arusha na maeneo jirani kutumia fursa hiyo kupata huduma za kisheria, huku akieleza kuwa Mahakama iko tayari kutoa ushirikiano wakati wowote utakapohitajika.
Vilevile, Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali nchini, Bonaventure Mwambaja, amesema mawakili hao wataendelea kuenzi kaulimbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayosisitiza kuwa haki ni haki ya kila Mtanzania.
Wakili Mwambaja amesema mawakili wa Serikali wana nafasi na mchango mkubwa katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi wote bila upendeleo wala ubaguzi, hatua inayochangia kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya taifa.


Post a Comment